Zitambue Hifadhi Za Taifa Ukanda Wa Kusini Mwa Tanza


 Leo nimependezwa tujifunze zaidi kuhusu hifadhi za taifa za ukanda wa Kusini, vivutio vingine vilivyopo lakini vikwamishi au changamoto zinazozikabili na hivyo kupelekea kuwa na watalii wachache na baada ya hapo tuzijue hatua ambazo zikifuatwa zitasaidia kuinua utalii ukanda huu wa Kusini;-

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotembelewa na watalii wengi sana kutoka pande zote za dunia. Wageni wengi ambao wanaingia huja kufanya utalii wa wanyamapori hasa ambao wapo kwenye hifadhi za taifa (TANAPA) na mara chache hufanya kwenye mapori ya akiba kutokana na miundo mbinu kutokuwa imeimarishwa mfano mahoteli, barabara na ofisi pia ambazo nyingi zipo nje na mbali ya maeneo hayo. TANAPA ni taasisi inayosimamia shughuli zote kwenye hifadhi za taifa kama ulindaji na mambo ya usalama wa watalii pamoja na wanyama pia kufanya matangazo na kuongeza wawekezaji ndani ya hifadhi hizi. Kwa sasa Tanzania ina jumla ya hifadhi za taifa 22 zilizogawanyika katika kanda kuu nne ya kusini mfano inapatikana hifadhi ya taifa Ruaha na Milima ya Udzungwa, Kaskazini inapatikana hifadhi ya taifa Ziwa Manyara na Tarangire, Magharibi inapatikana hifadhi ya taifa ya Katavi na Milima ya Mahale na kwa kanda ya Mashariki ipo moja tu ambayo ni hifadhi ya taifa ya Saadani.

Kwa makala yetu ya leo tutajifunza na kufahamu zaidi ukanda wa kusini wa watalii katika hifadhi zetu za taifa. Ukanda huu wa kusini hifadhi zake zinapatikana kusini mwa Tanzania ambazo zipo nne, hifadhi ya taifa ya Ruaha, Mikumi, Milima ya Udzungwa na hifadhi mpya ya Mwal. Nyerere (ambayo hapo zamani ilijulikana kama pori la akiba la Selous).


Ramani 1; kielelezo hichi cha ramani kinaonyesha hifadhi kuu nne za taifa za ukanda wa kusini ambazo ni hifadhi ya taifa ya Ruaha, Mikumi, milima ya Udzungwa na hifadhi mpya ya taifa ya Nyerere, zenye kutegemea sana watalii ambao wanapitia jiji la Dar es salaam hasa kwa uwanja wa ndege wa taifa wa Mwal. Nyerere.

Hifadhi ya taifa ya Ruaha;

Eneo hili liliteuliwa na kuwa hifadhi ya taifa ya Ruaha kutoka pori la akiba la Saba mwaka 1964, ambapo eneo kubwa inapatikana mkoa wa Iringa na Mbeya. Ni hifadhi yenye utajiri mkubwa sana wa wanyamapori kwa ujumla hasa makundi makubwa ya tembo na wenye umbo kubwa kulingana na takwimu za utafiti uliofanyika mwaka 2014 na kugundua ‘Rungwa-Ruaha ecosystem’ ndiyo yenye makundi makubwa na idadi kubwa ya tembo nchini. Pia ni eneo linalohifadhi idadi kubwa ya simba kiasi ambacho inachangia 10% simba waliobakia duniani, lakini pia lina idadi kubwa ya wanyama wengine wanaokula nyama kama chui, duma, fisi na mbwa mwitu ambao wapo hatarini kutoweka. Na wakati huo huo imejipatia umaarufu zaidi kwa kuwa na idadi kubwa ya tandala wa kubwa na wadogo pamoja na na miti anina ya mibuyu yenye umri mkubwa.

Hifadhi ya taifa ya Milima ya Udzungwa;

Eneo hili liliteuliwa kuwa hifadhi ya taifa kutoka kwenye hifadhi tano za misitu, mnamo mwaka 1992, likiwa linapatikana mkoani Morogoro na pia milima hii inaingia kwenye safu za milima ya Tao Afrika Mashariki (eastern arc mountains) yenye utajiri mkubwa wa spishi mbali mbali za viumbe pori. Misitu huu wa Hifadhi ya Milima ya Udzungwa inasadikika kuishi miaka milioni 30 na pia iliyokuwa imeungana na msitu wa Congo (congo basin) na Afrika magharibi lakini kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na shughuli nyingine za kibinadamu ikapungua na kubakia sehemu chache chache.

Hifadhi ya taifa ya Mikumi;

Eneo hili liliteuliwa na kuundwa hifadhi ya taifa mnamo mwaka 1964 ikiwa na jumla la kilomita za mraba 3230 na hivyo kuwa hifadhi ya taifa ya nne kwa ukubwa kabla pori la akiba la Selous kuwa hifadhi ya taifa (hifadhi ya taifa Nyerere). Pia hifadhi hii ni miongoni mwa hifadhi iliyopitiwa na barabara kuu ya Tanzania-Zambia, ikiwa inapakana na Selous upande wake wa kusini, Hifadhi ya milima ya Udzungwa na milima ya Uluguru. Eneo hili linasadikika kuendana na tambarare ya hifadhi ya taifa ya Serengeti, pia kwa maelezo ya wenyeji wa eneo hili wanasema ni rahisi kuona simba wanaopanda miti mikubwa kuliko wale wa hifadhi ya taifa ya ziwa Manyara.

Hifadhi ya taifa ya Nyerere (eneo lililojulikana kama pori la akiba la Selous);

Eneo hili liloianzishwa mwaka 1922 kama Pori la Akiba na mapema mwaka 2019 liliteuliwa na kuwa hifadhi ya taifa ya Nyerere ikiwa na ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 50000 hivyo kuwa hifadhi ya kwanza kwa ukubwa Afrika mashariki. Eneo hili pia lilitengwa na UNESCO 1982 kama lenye urithi wa dunia (world heritage site) kutokana na uwepo wa wanyama wengi tofauti tofauti na pia kama eneo ambalo halijaharibiwa. Na wanyama hao ni pamoja na tembo wa msituni, faru weusi, mbwa mwitu, twiga, punda milia na mamba. Japokuwa inatabiriwa kuathirika kwa wanyama na wenyeji wa eneo hilo hasa pale uchimnbaji wa bwawa la umemne utakapokamilika (stiegler’s gorge hydroelectrical power station) mwaka 2022.

Ukanda huu wa hifadhi za taifa za kusini, una vivutio vingi vya utalii ukiachana na wanyamapori waliopo kwenye hifadhi za taifa pia kuna wanyamapori waliopo kwenye mapori ya akiba mfano Mpanga-Kipengele, misitu ya asili na yenye historia za makabila kama msitu wa Nyumba nitu mkoani Njombe, vivutio vya kihistoria kama bonde la Isimila, Kalenga kwenye fuvu la chifu Mkwawa, majengo ya wakoloni ambayo wametawanyika sana mjini Iringa na baadhi ya sehemu za mkoa wa Njombe na Mbeya, daraja kimaajabu daraja la Mungu lililopo mkoa wa Mbeya, maji moto, pia ziwa Nyasa ambalo hutumika kama mpaka wa Tanzania na Malawi.

Kanda hii imekuwa ikipokea watalii wachache sana ukilinganisha na hifadhi za taifa zinazopatikana ukanda wa kaskazini ambazo ni hifadhi ya taifa ya Serengeti, Arusha, Tarangire, Mlima Kilimanjaro, Ziwa Manyara, na Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro. Uchache huu wa watalii umesababishwa na umbali ambao upo wa kutoka hifadhi moja kwenda nyingine kwa hizi za ukanda wa kusini pia umbali ambao upo kutoka kwenye jiji kubwa la katikati ambalo ni Dar es salaam mpaka kuzifikia hifadhi hizi pana urefu mkubwa, miundo mbinu bado ni duni mfano kuifikia hifadhi ya taifa ya Ruaha kutoka Iringa mjini ni mwendo wa masaa mawili kwenye baranbara ya vumbi, hivyo inakuwa ngumu sana kufikiwa na watalii hasa wasio na uwezo wa kutumia ndege kutoka uwanja mkubwa wa ndege wa Dar es salaam, bado ukanda huu hauna muamko wa shughuli za kitalii hivyo kumechangia hata wawekezaji kusita kujenga na kufungua mahoteli na majengo mengine ya kitalii. Pia, hifadhi nyingi za ukanda wa kusini zimeanzishwa baada ya uhuru wa nchi yetu Tanganyika na muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania hivyo hazikufahamika sana kwa kipindi kile cha wakoloni ukilinganisha na za ukanda wa kaskazini ambazo zilianzishwa kabla ya uhuru mfano hifadhi ya taifa ya Serengeti iliyoanzishwa 1959 hivyo wakoloni waliweza kuzibeba mioyoni mwao na kwenda kusimulia uzuri wa hifadhi hizo kwa ndugu zao waliporudi makwao.

Hivyo basi, kwa nia moja ya dhati na mapenzi makubwa niliyonayo kwa ukanda huu wa kusini wenye vivutio vingi vya kitalii na ambao bado mazingira yake mengi hayajabadilishwa na binadamu. wizara ya mali asili na utalii inayosimamia mali asilia za taifa letu, TANAPA taasisi inayosimamia hifadhi hizi, makampuni yanayo shughulika na utalii yanayokaribisha na kuunganisha hifadhi zetu na watalii na wadau mbali mbali wa sekta ya utalii kwa ujumla pasipo kusahau jamii zinazoishi jirani na hifadhi za taifa za ukanda wa kusini na kwa hifadhi zote kwa ujumla. Napenda kuainisha baadhi ya njia na hatua maalum ambazo zitakuza na kuongeza idadi ya watalii ukanda huu wa kusini endapo zitafatwa na kutekelezwa, ambazo ni;-

Kuboresha na kuimarisha miundo mbinu karibu na hifadhi hizi na ndani ya hifadhi zenyewe. Mfano kuimarisha barabara kutoka barabara ya vumbi inayotumia muda mrefu kufikia hifadhi ilipo na kuweka rami hivyo kusaidia na kuwezesha usafiri wa haraka kwa watalii na wafanyakazi kwa ujumla. Pia kuimarisha viwanja vya ndege ngazi ya mkoa mpaka viwanja vidogo vya ndege vinavyopatikana hifadhini ndani hivyo kuvuta idadi kubwa ya watalii wanaotumia anga na nchi kavu pia. Na kwa kufanya hivi kutasaidia kupunguza mwendo uliokuwa mrefu kutoka hifadhi moja mpaka nyingine na kutumia muda mchache.

Kutangaza, kufufua, kuboresha na kuimarisha vivutio vyote vya kihistoria na asilia vinavyopatikana ukanda wa kusini hivyo kuongeza vituo vingi hasa katika kusafiri hifadhi moja na kwenda nyingine na kupitia hivyo kunapunguza uchovu na urefu wa safari. Mfano ile ya kutoka hifadhi ya taifa ya Mikumi na Milima ya Udzungwa kuifikia hifadhi ya taifa ya Ruaha inayogharimu masaa si chini ya nane, kwa kuboresha na kuimarisha barabara za kufikia Isimila kwenye mabaki ya mawe yaliyotumiwa na watu wa kale (kipindi cha zama za mawe) pia Kalenga kwenye historia ya chifu Mkwawa wa kabila la wahehe wenyeji wa mkoa wa Iringa, na pia majengo yenye historia hasa kwa kipindi cha vita ya Mkwawa na Wajerumani yaliyopo Iringa mjini. Hivyo kwa kutangaza na kufufua vitutio hivi itasaidia ongezeko kubwa la watalii.

Kuandaa maonyesho mbalimbali yanayohusu tamaduni nyingi za watu wa kusini mfano kuandaa maonyesho ya kushindanisha ngoma, ufumaji, ususi, mavazi, vyakula, historia ya kila kabila. Hivi vyote vikidumishwa, kuandaliwa na kutekelezwa hasa kipindi cha watalii wengi wanavoingia ukanda huu itasaidia kuongeza pato la taifa kupitia viingilio vitakavyo kubalika, kuongeza wawekezaji kuongeza ajira na idadi kubwa ya watalii na makazi ya watu kwa ujumla.

Kubuni sehemu nzuri na kujenga jumba la utalii la ukanda wa kusini aidha lijengwe mkoani Iringa, Morogoro au Dodoma kuliko kuendelea kutumia jiji la Dar es salaam kama ndio jiji la katikati kwa hifadhi za taifa za ukanda wa kusini. Na ndani ya jumba hilo kuwe na taarifa zote za shughuli za kiutalii, vivutio vyote vya wanyama pori hasa hifadhi za taifa, vivutio vya kihistoria, tamaduni na mila za watu wa kusini pasipo kusahau makampuni yote ya utalii ili kurahisisha shughuli za kiutalii na kumsaidia mtalii kuchagua aanze na kivutio kipi.

Kubuni bidhaa inayouzika sana dunia inayozalishwa zaidi ukanda wa kusini mwa Tanzania na kuipa jina mojawapo ya hifadhi za ukanda huu hivyo kurahisisha kufahamika, kuuzika na kujipatia umaarufu wa hifadhi hiyo. Mfano jinsi ambavyo hifadhi za kaskazini zinajipatia umaarufu kupitia vinywaji kama bia ya Serengeti na Kilimanjaro zimeipa kanda ya kaskazini umaarufu sana hivyo imesaidia ongezeko kubwa la watalii.

TANAPA pamoja na wizara ya mali asili na utalii kwa ujumla ipunguze vibali kwa wawekezaji wa mahoteli na makampuni ya utalii hasa katika kipindi hiki cha kuinua utalii kusini. Hii itasaidia ongezeko kubwa la utalii kulingana na kwamba kutakuwa na hoteli zenye hadhi tofauti tofauti na makampuni mengi yenye uzoefu tofauti katika kuhudumia watalii wa hadhi mbalimbali.

Kuelimisha zaidi jamii za watu wa ukanda wa kusini kuhusu shughuli zote za utalii kama maduka ya vitu asilia, mavazi pamoja na vyakula na vinywaji hivyo kuweza kupata muamko mkubwa. Pia kuwasisitiza sana juu ya maswala mazima ya Amani na utulivu kwa maeneo yote nchini na kuwa wepesi kutoa taarifa panapotokea wageni wasioeleweka na kuaminika kwani shughuli za kiutalii pasipo Amani na utulivu ni hadithi za kufikirika.

Zitambue Hifadhi Za Taifa Ukanda Wa Kusini Mwa Tanza Zitambue Hifadhi Za Taifa Ukanda Wa Kusini Mwa Tanza Reviewed by cmakigo on January 08, 2021 Rating: 5

No comments:

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
Powered by Blogger.