Msitu Wa Nyumbanitu: Msitu wa ajabu mkoani Njombe wenye kuku weusi, ng'ombe weusi, mbuzi weusi na kondoo weusi
Njombe ni mmoja wa mikoa 31 ya Tanzania, uliorasimishwa kuwa mkoa mwaka 2012 mara baada ya kutenganishwa na Iringa inayopatikana Nyanda za Juu kusini Kwa Tanzania. Hapo awali Njombe ilikuwa ni wilaya ndani ya mkoa wa Iringa ikiwa ina ukubwa wa eneo la mraba la Km 21,347. Sensa ya mwaka 2012 ilionesha kuwa Njombe ina wakazi wanaofikia kuwa 702,097. Mkoa wa Njombe ni maarufu kwa kilimo cha mahindi na viazi.
Makabila makubwa ya wenyeji mkoani Njombe ni Wabena, Wakinga na Wapangwa, na uwiano wao ni 37:11:3.
Kama ilivyo mikoa mingine, Njombe ina historia yake ya kipekee. Neno "Njombe" lenyewe limetokana na jina la mti unaoitwa "Mdzombe" ambao ulipatikana kwa wingi eneo la Mdandu yalikokuwa makao makuu ya Ngome ya Mjerumani wakati huo (Bomani). Mkoa wa Njombe Una vivutio vingi sana vya utalii, Nyumbanitu ni kimojawapo.
NYUMBANITU NI NINI?
Neno "Nyumbanitu" ni muunganiko wa maneno mawili; nyumba na nitu. Neno "Nitu" manaake ni Giza au Nyeusi. Hivyo Nyumbanitu maana yake ni nyumba yenye Giza au nyumba nyeusi.
Nyumbanitu si nyumba kama lilivyo neno lenyewe, bali ni msitu mdogo wenye ukubwa wa hekta mbili na nusu (2.5) tu. Msitu huu mdogo wenye mambo ya kustaajabisha upo katika Kijiji cha Mlevela, Kata ya Mdandu Wilaya ya Wanging’ombe, ni Km 15 kutoka Njombe mjini.
Kwa sasa msitu huo unatunzwa na wanandugu , Julius Vangameli Msigwa na Alex Vangameli Msigwa, ambao kabla ya kutembeza wageni msituni huwa lazima waulize nia ya ujio wa wageni husika. Kuna ambao huenda nyumbanitu kuomba mizimu iwape baraka Katika mambo yao. Kuna ambao huenda kuchuma dawa, wengine huenda kujifunza Mila na desturi za mahali hapo nk.
Kabla ya kuingia ndani ya msitu huo mdogo ni lazima wenyeji (Familia ya Msigwa) ambao ndio wenye msitu wao wafanye maombi mafupi Kwa mizimu ili wapate ruhusa ya kuingia. Si kila mahali unaweza kutumia kuingia ndani ya msitu huo, kuna njia maalumu ambayo Si rahisi kuijua, labda wenyeji tu.
Iwapo utathubutu kuingia ndani ya msitu huo bila kibali cha familia iliyopewa jukumu la kuulinda, itakuwia vigumu kutoka. Utatembea Sana ndani ya msitu bila kuiona njia ya kutokea. Na kuna uwezekano mkubwa wa kufia humo labda tu wenyeji wakunusuru Kwa kuiomba mizimu ikuachie.
Mita kadhaa baada ya kuingia ndani ya msitu huo utaona sehemu ya mapokezi ambayo huwa pana vyungu vyeusi vyenye umri mkubwa sana, vingine vikiwa vina maji ya mvua na vingine vikiwa na unga wa mtama. Utaona pia vigoda, mkuki, tunguli, vibuyu, mti uliovishwa kaniki, nyungo na sarafu za zamani sana. Hivi vyote hutumika wakati wa zoezi la tambiko. Vifaa hivyo vyote vinadhaniwa kuwa mahali hapo tangu karne ya 14 au 15.
Maajabu ya msitu huo ni uwepo wa kuku weusi wenye midomo myekundu ambao wahifadhi wanasema kuwa kuku hao hawazeeki, hawafugwi na wala hawaliwi. Kuku hao huonekana kwa wingi wakati wa mavuno na inapofika masika, hawaonekani tena. Kuku hao wakitoka nje ya msitu, hakuna mwanakijiji ambae anaweza kuwakamata.
Inasemekana pia kuna ng’ombe, mbuzi na kondoo weusi ambao huingia kwa msimu ndani ya msitu huo bila kujua ni wapi hasa wametokea. Wanyama hawa waliingizwa kwa mara ya kwanza miaka mingi sana huko nyuma. Waliletwa mahali hapo kama adhabu kwa wale ambao walikiuka utaratibu wa kimila, badala yake wakaambiwa wapeleke aina hiyo ya wanyama na ndege ili wasamehewe makosa yao. Mpaka Leo hii, ndege (kuku) na wanyama hao (ng'ombe, mbuzi na kondoo) hawazeeki, hawaliwi wala kuchungwa na yeyote. Hata kuonekana kwa viumbe hawa kumekuwa ni kwa msimu tu.
Kuna nyakati, kila ikifika asubuhi, kuna sauti ya kengere za ng'ombe kutoka ndani ya msitu huo kuashiria kuwa ng'ombe wanaamka na kuelekea malishoni, na ikifika jioni pia sauti ile hujirudia kuashiria kuwa ng'ombe wanarudi kutoka malishoni japo hawaonekani wakitoka.
Ndani ya msitu huu kuna rupia ambazo huwa zinawavutia wengi na hivyo kuingiwa na hamu ya kuziiba, lakini kimaajabu hujikuta wakishindwa kutoka ndani ya msitu hadi pale wenyeji wanapoamua kuwanusuru.
Kuna mapango makubwa ambayo watu zaidi ya mia wanaweza kuishi, huku simulizi zikieleza kwamba mapango hayo yalitumika kujificha wakati wa vita, ni pale ambapo Chifu Mkwawa alivamia maeneo hayo. Si tu mapango hayo yalitumika kujificha dhidi ya uvamizi wa Chifu Mkwawa, vilevile yalitumika kujificha wakati wa vita ya Majimaji iliyopiganwa na makabila mbalimbali dhidi ya Mjerumani mwaka 1904---1907. Mapango hayo yana giza totoro na vijito vya maji yanayotiririka.
Si ruhusa Kwa wanawake walio katika siku zao, yaani kwenye hedhi kuingia ndani ya msitu huo. Ni mwiko kabisa, na ikiwa mwanamke atajidanganya kufanya hivyo, basi miaka yake yote atabaki akitokwa na damu ya hedhi bila ukomo na hakuna dawa ya kumtibu.
Wanawake wajawazito pia hawaruhusiwi kuingia. Marufuku hii imeandikwa kwenye ubao maalumu nje kabisa ya msitu huo mdogo. Ili kuhakikisha kuwa wageni (watalii) hawakiuki marufuku hiyo, mwenyeji huirudia marufuku hiyo kwa mdomo ili kutilia mkazo.
Sharti jingine kabla ya kuingia msituni humo ni kuvua viatu, kofia na vilemba. Baada ya kufuata taratibu zote, mwenyeji (Mzee Julius Vangameli Msigwa) huomba ruhusa ya kuingia msituni kwa kuongea maneno ya kibena;
“Hodi! Hodi Mutwa! Avagenzi ava vanuhile! Vihwandza...(hutaja lengo la ujio)! Hodi vamkongwa, Hodi vamwafute! Hodi Vakiswaga!....twisuka mwanuhile avagenzi ava,”
Baada ya maneno haya, mwenyeji huruhusu watu waingie wakiwa kwenye mstari mmoja mnyoofu. Mara nyingine wageni huambiwa waingie kinyumenyume kwanza na kisha wageuke kawaida, na hata muwapo ndani ya msitu huo hamruhusiwi kushika matawi ya miti inayoziba njia, badala yake mnatakiwa kuinama ili kuikwepa na si kuishika.
Kama ni msimu wa kiangazi, basi utawaona kuku weusi ndani ya msitu, wakiwa bize na kujitafutia chakula. Utaiona mimea ya kipekee ambayo imekuwepo hapo kwa zaidi ya karne mbili. Utashuhudia mapango yenye kutiririsha maji ndani yake huku yakiwa na giza totoro.
Wenyeji wa eneo hili na vijiji vya karibu wamekuwa wakitumia msitu wa nyumbanitu kufanya tambiko la kuomba mvua iwapo mvua haijanyesha kwa muda mrefu kipindi cha masika. Zoezi la tambiko huambatana na kuchinja ng'ombe kama kafara ya tambiko hilo. Mara baada ya tambiko wenyeji hujiandaa kuipokea mvua kubwa mno ndani ya muda mfupi. Kujilinda na mvua hiyo, watambikaji huenda na makoti makubwa au miamvuli, maana mvua haijawahi kutokunyesha baada ya tambiko.
Mwaka 1940 eneo hili la nyumbanitu lilikuwa likimilikiwa na Chief Mbeyela ambae alikuja kuliuza eneo hili kwa Wazungu waliotaka kulima chai. Ni wazungu waliokuwa wanamiliki kampuni iitwayo Tanganyika Wattle Company (TANWAT). Baada ya kununua eneo hili, Chief Mbeyela aliwapa sharti la kutunza eneo hili dogo la nyumbanitu ambalo lilikuwa ndani ya eneo kubwa zaidi lililonunuliwa na wazungu. Wazungu hawa walikubali lakini baadae wakakiuka sharti kwa kukata miti yote ya eneo hili la nyumbanitu ili wafanye shughuli zao za mazao. Asubuhi ya siku ya pili baada ya kukata miti yote ya eneo hili, walikuta pako vilevile kana kwamba zoezi la siku iliyopita ilikuwa ni ndoto tu. Miti yote ilirudi kama ilivyokuwa awali.
Wazungu walivyoona hivyo, wakachukua uamuzi wa kuchoma moto eneo hilo la nyumba nitu. Zoezi lilifanikiwa. Masika ilipofika, hakuna mvua iliyonyesha mpaka kiangazi kilipokaribia. Wazee wa kijiji wakaamua kuwafuata wazungu ili kuwaambia chanzo cha ukame wa mwaka huo. Suluhisho la ukame huo lilikuwa ni wazungu kukabidhi kaniki, kuku mweusi na ng'ombe mweusi ili wasamehewe kosa lao. Wazungu wakakabidhi vitu hivyo na tambiko likafanyika. Muda mfupi tu baada ya tambiko, mawingu yakasogea na mvua kubwa ikaanza kunyesha. Hapo ndipo eneo hilo likaendelea kuheshimiwa zaidi.
Miaka ya baadae Chifu wa wabena, Mkongwa aliwaita wanae watatu na kuwakabidhi majukumu kulingana na uwezo wa kila mmoja.
Chifu Mkongwa alisoma tabia za watoto wake kisha akawakabidhi majukumu.
Mtoto wa kwanza aliitwa Fute, alipewa jembe kama ishara ya kuwa mkulima hodari, akitakiwa kuhakikisha anasimamia shughuli za kilimo ili kuepuka janga la njaa.
Mtoto wa wapili aliyeitwa Mkongwa alikabidhiwa mkuki kama ishara ya kupewa ruhusa ya kupambana na maadui, huku akipewa kazi ya utawala.
Mtoto wa mwisho alikabidhiwa ungo kwa maana ya kuwa mganga wa jadi. Huyu ndiye aliyepewa jukumu la kufanya matambiko na kuongoza vikao vyote vya kimila.
Mtoto huyo ndiye aliyepewa kazi ya kuulinda na kuutunza msitu huo. Zana zote walizokabidhiwa watoto hao zimehifadhiwa ndani ya msitu huo hadi leo na ndizo zinazotumika kuoneshwa kwa wageni. Zoezi la kurithishana utunzaji wa msitu limeendelea mpaka Leo hii ambapo familia ya Julius Msigwa ina jukumu hilo.
Mwaka 1993, waumini fulani wa makanisa ya kikristo (walokole) walienda nyumbanitu ili wafanye maombi ya kuvunja nguvu zote za giza za eneo hilo bila kufuata taratibu za kimila kwa imani kuwa chanzo cha mikosi na matatizo ya watu wa eneo hilo ni uwepo wa nyumbanitu. Baada ya maombi ya siku nzima, waumini hao walishindwa kutoka ndani ya msitu huo. Badala yake wakaanza kupiga kelele kuomba msaada. Wakiwa ndani ya msitu walipotea njia ya kutokea nje. Wasamalia Sema wakaenda kutoa taarifa kwa wazee ili walokole hao wanusurike na madhira hayo.
Zoezi la maombi ya walokole lilisababisha kukosekana kwa mvua kipindi cha masika baada ya mizimu ya mahali hapo kuchukia.
Ili kurudisha mvua, waumini wote waliohusika na maombi hayo, waliitwa ili waombe msamaha kwa mizimu kwa kuleta kaniki, kuku mweusi, ng'ombe mweusi na sarafu ambazo waliiba mahali hapo. Waumini hao walitii agizo hilo la wazee na zoezi la kuomba msamaha kwa njia ya tambiko likafanyika. Haukupita muda mrefu mvua kubwa ikaanza kunyesha kama ishara ya kusamehewa makosa yao.
Mpaka muda huu naandika makala hii, nyumbanitu ipo na inatembelewa na wageni wengi kwa sababu mbalimbali. Karibu mkoa wa Njombe ujionee mwenyewe nyumbanitu na vitutio vingine kama Makaburi ya mashujaa wa Kibena, Mawe ya ajabu, Majengo ya kale ya wajerumani, Maporomoko ya maji ya Luhaji, mashamba makubwa ya chai nk.
Sapoti utalii wa ndani, tuna mengi yakujifunza na kutuburudisha share na nawengine.
No comments:
Post a Comment