vijana wahimizwa kuchangamkia fursa ya ufugaji samaki katika mabwawa

 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewahimiza vijana kujihusisha na ufugaji wa samaki katika mabwawa huku akisema fursa hiyo itawaokoa vijana wengi kuondokana na kilio cha ukosefu wa ajira nchini.

Gekul aliyasema hayo alipotembelea Kampuni ya ufugaji wa Samaki inayojulikana kwa jina la Bigfish iliyopo Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Januari 6, 2021.

Alisema kuwa muelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa samaki katika mabwawa kwasababu uvuvi wa kutegemea maji ya asili umekuwa mkubwa na kupelekea kupungua kwa rasilimali za uvuvi, hivyo kimbilio pekee ambalo litawawezesha vijana wengi kupata ajira ni ufugaji wa samaki katika mabwawa.

Aliongeza kuwa Serikali ipo mbioni kuweka miongozo na kanuni za ufugaji huo ili kuwalinda na kuwawezesha wafugaji waweze kufuga vizuri na kwa kuzingatia taratibu zitakazowekwa.

“Serikali itawawezesha vijana kwa hali ya juu, kuwajengea mabwawa, kuwapatia mafunzo ya ufugaji bora wa samaki ili vijana wetu waweze kujikwamua na suala la ukosefu wa ajira,” alisema Gekul

Aliendelea kusema kuwa Rais, Dkt. John Magufuli aliahidi ajira zaidi ya milioni 8, moja ya sekta ambayo inategemewa kutengeneza ajira hizo ni ya uvuvi hivyo aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kujikomboa kiuchumi.

Kuhusu uwezeshaji, Gekul aliziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 10 katika mapato yao kwa ajili ya kuwawezesha vijana na watu wenye Ulemavu ili waweze kufanya ufugaji katika mabwawa na kujipatia ajira.

Aidha, Gekul alisema kuwa anafahamu changamoto zinazokabili ufugaji wa samaki wa mabwawa ni pamoja na uhaba wa vifaranga vya samaki na ukosefu wa chakula cha kutosha na cha uhakika kwa ajili ya samaki hivyo alitumia fursa hiyo kuiagiza Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kutafuta muarobaini wa changamoto hizo ili kuwaondolea kero hiyo wafugaji.

Aliongeza kuwa ufugaji wa samaki katika mabwawa utasaidia kupunguza kilio cha uhaba wa malighafi unaokabili viwanda vingi nchini huku akiongeza kuwa ufugaji huo pia utasaidia kupunguza uvuvi haramu kwa sababu watu watakuwa na chanzo mbadala cha kujipatia kipato.


vijana wahimizwa kuchangamkia fursa ya ufugaji samaki katika mabwawa vijana wahimizwa kuchangamkia fursa ya ufugaji samaki katika mabwawa Reviewed by cmakigo on January 07, 2021 Rating: 5

No comments:

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
Powered by Blogger.