Rais wa Zanzibar awataka wanafunzi kusoma kwa bidii na nidhamu

 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wanafunzi kutumia vyema fursa za kuwepo miundombinu bora ya masomo  kwa kusoma kwa bidii na nidhamu.


Dk. Mwinyi amesema hayo leo katika Ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Hasnuu Makame , iliopo Kibuteni Mkoa Kusini Unguja.


Amesema wanafunzi watakaopata nafasi ya kusoma katika skuli hiyo wanapaswa kutumia vyema fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii, ili waweze kufaulu katika amsomo yao badala ya  kujihusisha na masuala yatakayosababisha kuharibikiwa katika maisha yao ya baadae.


Alisema ni matumaini yake kuwa wanafunzi watakaosoma skuli hiyo watafulu vyema katika mitihani yao ya Taifa, kw akuwa   skuli hiyo iko katika mazingira mazuri, walimu wazuri pamoja na kuwa na vifaa vya kutosha.


Aidha, aliwataka wakuu wa Wilaya na mikoa kushirikiana na wananchi ili kufanikisha wanafunzi wote watakaotoka katika skuli 34 za Sekondari mkoani humona kujiunga katika Skuli hiyo wanafaulu vizuri.


Vile vile aliwataka walimu kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa kusomesha vizuri pamoja na wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao ili kubaini chanagmoto zinazoweza kujitokeza.


Kuhusina na ujenzi wa majengo hayo, Dk. Mwinyi alisema anaridhishwa na ubora wa majengo yaliopo katika skuli hapo, na akasisitiza kuwa kuanzia sasa Serikali haitovumilia kuona inakuwepo miradi inayojengwa chini ya kiwango.


“Miradi itakayojengwa chini ya kiwango sasa basi, lazima matumizi ya fedha yaendane na thamani hali ya majengo, tutamchukulia hatua kiongozi yoyote atakejinufaisha kupitia miradi ya Serikali”, alisema.


Aliahidi kushirikiana na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi (BADEA) pamoja na kumpongeza Mkandarasi wa ujenzi huo Kampuni ya RUINS  kwa kazi kubwa na nzuri ya kukamilisha ujenzi wa majengo hayo.


Aidha, aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kusimamia vyema miradi ya elimu, sambamba na kuitaka kujenga viwanja katika eneo la skuli hiyo ili wanafunzi wapate fursa ya kucheza pamoja na kuagiza eneo la skuli hiyo kupimwa ili kuzuia uvamizi wa ardhi.


Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alipongeza juhudi kubwa zilizofanya na Serikali za Awamu ziliotangulia, akibainisha kazi kubwa imefanyika kuinua kiwango cha elimu nchini.


Alitoa pongezi maalum kwa Uongozi wa Serikali ya Awamu ya saba chini ya Dk. Ali Mohamed Shein kwa juhudi kubwa za kuinua sekta ya elimu nchini, ikiwemo ujenzi wa majengo ya ghorofa, ununuzi wa madawati, kuongeza idadi ya walimu, kuondoa michango kwa wanafunzi, kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu pamoja na kukiimarisha Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).


Alisema kwa kutambua umuhimu kwa maendeleo nchini, Serikali itaendelea na juhudi za kuyafanyia matengenzo majengo ya skuli pamoja na kujenga mapya, kuongeza upatikanaji wa vifaa, kupitia upya mitaala ya elimu pamoja na kuzingatia maslahi ya walimu, ikiwa ni hatua ya utekelzaji wa Ilani ya CCM. 


Aidha, Dk. Mwinyi aliridhia Skuli hiyo kuitwa jina la ‘Hasnuu Makame Secondary school’ kama ilivyopendekezwa.


 Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohamed Said alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi kuzingatia umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika maendleeo ya elimu ya watoto wao.


Nae, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhandisi Dk. Idrissa Muslim Hija alisema  ujenzi wa skuli hiyo umefanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Kiuchumi (BADEA) na kugharimu Dola za Kimarekani Milioni 6.6.


Alisema  ujenzi huo unahusisha Majengo mbali mbali, ikiwemo jengo la Utawala, Dakhalia, nyumba za walimu pamoja na madarasa.


Alieleza kuwa jengo la Dakhalia lina jumla ya vyumba 38 likiwa na uwezo wa kukaliwa na wafunzi 152, wakati ambapo kuna madarasa 16 yenye uwezo wa kutumia na wanafunzi 640, ikiwa ni wastani wa wanafunzi 40 kwa darasa moja,


Alisema miongoni mwa chanagmoto zinazoikabili Skuli hiyo, ni pamoja na ukosefu wa uzio pamoja na Kampuni ya RUINS kuidai Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali kiasi cha shilingi Milioni 541.7 ikiwa sehemu ya malipo ya Ujenzi wa jingo la Dakhalia ya wanaume.


Dk. Idrissa aliwataka wananchi wote wanaozunguka eneo hilo kushirikiana katika kulinda rasilimali za skuli hiyo kwa faida ya vizazi vijavyo.


Katika hafla hiyo Viongozi mbali mbali wa Kitaifa walihudhuria, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla, Makamo wa Pili wa Rais mstaafu Balozi Seif Ali Idd, Katibu wa Baraza la  Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Katibu Mkuu wa CCM Abdalla Juma Sadalla, Mawaziri pamoja na wananchi wa shehiya mbali mbali za Mkoa Kusini Unguja.

Rais wa Zanzibar awataka wanafunzi kusoma kwa bidii na nidhamu  Rais wa Zanzibar awataka wanafunzi kusoma kwa bidii na nidhamu Reviewed by cmakigo on January 11, 2021 Rating: 5

No comments:

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();
Powered by Blogger.